Utamu wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL), msimu wa 2017/18 utaanza rasmi kesho Jumamosi
Agosti 26, 2017 kwa michezo saba itayochezwa katika viwanja tofauti
nchini.
Mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba watashuka
kwenye Uwanja wa Uhuru kuwakaribisha Ruvu Shooting kesho Jumamosi,
wakati mabingwa watetezi Yanga kesho kutwa Jumapili itakuwa kwenye
uwanja huo kukaribisha Lipuli iliyorejea Ligi Kuu baada ya kusubili kwa
miaka zaidi ya kumi.
Simba itaingia katika mchezo huo
ikiwa na kikosi chake chenye thamani ya Sh 1bilioni wakiwa na lengo moja
tu kuthibisha ubora wao na kuonyesha mashabiki na wapenzi wao kuwa
msimu huu wataupata ubingwa.
Safu ya ushambuliaji wa
Simba chini ya Mganda Emmanuel Okwi bado haijafanya kila kilichotegemewa
na wengi hivyo watawajibika kuhakikisha wanafunga mabao mengi dhidi ya
Ruvu Shooting na kutuma salamu kwa timu nyingine.
Mabingwa
wa Kombe la Mapinduzi, Azam wenyewe watakuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda
Sijaona mjini Mtwara kuwavaa wenyeji Ndanda FC iliyokuwa na maandalizi
duni pamoja na kufanya usajili wa mafungu.
Azam
inayoundwa na vijana wengi pamoja na sura mpya itacheza mechi yake ya
kwanza ikiwa bila ya mshambuliaji wake John Bocco, kipa Aishi Manula na
beki Shomari Kapombe waliotimikia Simba, pia wakiwa na kumbukumbu mbaya
kila wanapocheza na Ndanda hivyo wanawajibu wa kuondoa jinamizi hilo.
Singida
United iliyopanda daraja kwa mara ya kwanza, lakini usajili wake na
uwekezaji mkubwa waliofanya unaifanya mechi yao ya kwanza dhidi ya
Mwadui FC kuwa na utamu wa pekee kwenye Uwanja Mwadui Complex,
Shinyanga.
Mabingwa mara mbili wa Ligi Kuu, Mtibwa
Sugar watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani kuwavaa Stand
United wakati Mbao watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba.
Majimaji itakayosafiri kuifuata
Mbeya City kwenye Uwanja wa ya Sokoine jijini Mbeya, huku wageni wengine
wa ligi hiyo Njombe Mji ikiialika Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye
Uwanja wa Sabasaba huko Makambako.
0 comments:
Post a Comment