MCHEZAJI
anayeongoza kwa kupendwa na mashabiki wa Simba, Emmanuel Okwi ametamka
kwa mdomo wake kuwa kiungo mpya wa Yanga, Kabamba Tshishimbi ni fundi na
anajua kazi yake.
Okwi amesema wazi kuwa kiungo huyo
mpya wa watani zao, anajua soka na kumvulia kofia kwa namna alivyokipiga
katika mechi ya Ngao ya Jamii juzi Jumatano pale Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.
Straika huyo aliyewahi kucheza
Yanga, alisema Tshishimbi anacheza soka la kazi, ushindani pamoja na
kuburudisha na kwamba kama hiyo juzi alishuka uwanjani akiwa hayupo fiti
kwa asilimia zote, hajui akiwa fiti atakuwaje kwa mpira mwingi
aliowapigia Taifa.
Katika mechi hiyo ambayo Yanga
ililala kwa penalti 5-4 baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana,
kiwango cha Mkongomani huyo kimemfanya Okwi aliyewahi kuifunga Yanga
mara tatu kuthubutu kutamka neno kutoka moyoni ambalo hata kocha wake,
Joseph Omog alilikubali.
“Tshishimbi ana uwezo mkubwa,
ameweza kucheza maeneo mengi, anajituma kuhakikisha timu yake inakuwa na
mafanikio. Uchezaji wa aina yake ni wa mchezaji mwenye kuona mbali,
hivyo wamepata mtu atakayewasaidia kwenye ligi na mashindano mengine,”
alisema Okwi.
Mbali na Okwi, kiungo fundi wa kuchezea
mpira, Haruna Niyonzima, naye alimzungumzia Tshishimbi na kumpa sifa
kwamba Yanga wamepata mtu ambaye walimtafuta kwa muda mrefu.
“Nashukuru
kwa kupata ushindi katika mechi yangu ya kwanza, ila nitoe pongezi kwa
kiungo mpya wa Yanga Tshishimbi, alikuwa kikwazo kikubwa kwetu na
pengine ndio alifanya tushindwe kupata ushindi ndani ya dakika tisini,”
alisema.
Kiungo mwingine wa Simba, Mghana James Kotei
naye alifunguka na kusema kuwa katika usajili ambao Yanga wameufanya
msimu huu, basi Mkongomani huyo ndiye fundi na atawabeba katika mechi
nyingi zilizopo mbele yao.
KIGOGO SIMBA AMZUNGUMZIA
Mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tulliy, alisema Yanga ilikuwa ife
katika mchezo huo, lakini uchawi wao ulibebwa na Tshishimbi ambaye kila
alipogusa mpira uwanja mzima ulizizima.
Bosi huyo
alisema Tshishimbi aliyesajiliwa na Yanga akitokea Mbambane Swallows ya
Swaziland, ameonyesha si mchezaji wa wasiwasi na anayajua majukumu yake
ingawa bado hajaiva katika mazoezi ya stamina akionekana kutokuwa na
mazoezi ya kutosha.
“Niseme ukweli pengine ndiyo
usajili mkubwa kwa Yanga ni mtu ambaye binafsi nimeridhika na kiwango
chake. Huyu ni kiungo wa kweli, anajua majukumu yake amewasaidia sana
Yanga katika kiungo chao, lakini naona kama bado hana mazoezi ya
kutosha,”alisema Tulliy
LWANDAMINA HUYU
Wakati
Tulliy na Wanasimba wengine wakimzungumzia kiungo huyo mwenye miaka 27,
kocha wa Yanga, George Lwandamina amesema Mkongomani huyo alionyesha
thamani ya kwamba kwanini viongozi wa Yanga walipania kumsajili, lakini
akasema bado kuna mengi yatakuja kutoka kwake.
Lwandamina
alisema alimtaka Tshishimbi kucheza kwa asilimia 70 tu katika mchezo
huo akihofia anaweza kuumia kutokana na kukosa mazoezi mazito, lakini
ana imani wana Yanga watafurahia zaidi utamu wa kiungo huyo.
“Huyu
ni mchezaji bora alikuwa ni kitu muhimu katika timu yetu nafikiri
amewapa faraja viongozi wa Yanga na mashabiki wao katika mchezo huu,”
alisema Lwandamina.
“Tulichelewa kumpata nafikiri
angefika mapema wakati tunaanza maandalizi angekuwa bora zaidi lakini
alichekewa ndiyo maana nilimtaka asicheze kwa kiwango kikubwa sana
angeweza kuumia”
0 comments:
Post a Comment