Monday 21 August 2017

PONDA AFUNGUKA JUU YA MAITI ZILIZOOKOLEWA BAHARINI



SIKU moja baada ya gazeti la Nipashe kuripoti kuhusu uwapo wa maiti 15 zilizoopolewa baharini mfululizo katika siku za karibuni zikiwa zimefungwa ndani ya viroba, mwanaharakati Sheikh Issa Ponda ametaka serikali kutoa kauli kuhusu jambo hilo.

Akizungumza na gazeti la  Nipashe kwa simu jana, Sheikh Ponda ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipaza sauti kuhusu uwapo wa mauaji ya raia kwenye mikoa ya kusini mwa Tanzania, lakini haijasikilizwa.

"Tunapongeza Nipashe kwa habari hii," alisema Sheikh Ponda kwa sababu "imefichua mambo mengi.",
"Haya tumeshayasema lakini hakuna aliyetusikiliza.

"Ni wakati mwafaka serikali ikatoa tamko kwa vile vyombo vya dola vimeonyesha kushindwa kueleza miili hiyo ni ya watu gani na inatoka wapi, (na kibaya) zaidi wanasema wanatambua miili mitatu iliyookotwa ambayo kwa sasa iko Muhimbili."

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu juzi kuwa miili iliyookotwa ni mitatu na haikuwa kwenye viroba.

Sheikh Ponda alisema mauaji hayo ni makubwa na hayajawahi kutokea kwa serikali zilizopita kwa miili kusambaa baharini na wavuvi kuiopoa.

Alisema jambo hilo si la kawaida, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa wala kutolewa taarifa ya kina na serikali kuhusu hali hiyo.

"Jumuiya inaona ni wakati mwafaka kwa serikali kutueleza kwa kuwa vyombo vya dola havijui au havitaki kutoa taarifa juu ya kile kinachoendelea hadi maiti kuokotwa zikiwa ndani ya viroba baharini," alisema.

Sheikh Ponda alisema kunapokuwa na masuala mazito kama hayo, kauli ya serikali inahitajika ili kujua ukweli na uhakika wa ulinzi kwa wananchi wake.

Wavuvi na wafanyabiashara katika masoko na minada ya samaki ya Kunduchi, Ununio na Feri jijini Dar es Salaam waliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki kuwa wanaishi kwa hofu baada ya kuopolewa miili 15 ya watu baharini ikiwa imewekwa katika mifuko maalumu kama viroba, Bara na Zanzibar katika siku za karibuni.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vilivyozungumza na Nipashe, miili hiyo iliokotwa kwa nyakati tofauti na wavuvi ambao waliwajulisha polisi, waliofika kuichukua.

Kuwapo kwa idadi kubwa ya miili inayoopolewa kutoka baharini au kukutwa fukweni ikiwa imefungwa kama mzigo kumefanya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kaskazini mwa wilaya ya Kinondoni kuingiwa na hofu pia.

Mwanaharakati huyo pia alirusha lawama kwa Bunge akidai kuwa chombo hicho cha kutunga sheria kimeshindwa kufanyia kazi barua yao ya Julai 14, mwaka huu, yenye kumbukumbu namba JTKT/BJMT/1/17 kuomba kuundwa kwa kamati huru ya Bunge, kufanya uchunguzi wa mauaji ya raia kwenye maeneo ya ukanda wa kusini.


"Tuliona kabisa haifai kutegemea taarifa za upande mmoja, yaani Jeshi la Polisi pekee, bali tuwe na chombo huru kitakachotokana na chombo cha uwakilishi wa wananchi, wakienda kuchunguza wataleta taarifa huru na kujua ukweli wa mambo," alisema na kueleza zaidi:

"Cha kusikitisha Spika hakujibu barua yetu kabisa.

"Tafsiri ya haraka ni kuwa uwakilishi wa wananchi kwenye chombo hicho uko wapi? Wito wetu uko palepale, jambo hili siyo la kuacha lipite bure, tunataka kuona hatua zikichukuliwa."

Nipashe ilimtafuta Spika Job Ndugai kuhusu lawana hizo za Sheikh Ponda dhidi ya Bunge, lakini simu yake ilikuwa haipatikani na hakujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) aliotumiwa.

KUOPOLEWA MIILI
Nipashe pia ilimtafuta Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, ambaye alikiri kuopolewa kwa miili kwenye fukwe za Bahari ya Hindi imefungwa kwenye viroba.

"Zipo maiti zimeopolewa na wavuvi katika Pwani ya Dar es Salaam, zikiwa ndani ya mifuko zimeshonewa ndani," DCI Boaz alithibitisha.

Alipoulizwa idadi na maeneo zinakotoka na zinakohifadhiwa, alisema: "Hilo waulize makamanda wa polisi wa mikoa ya kipolisi, siwezi kuwa na takwimu hizo."

Alisema zaidi: "Pia kuhusu zinatoka wapi ni mapema sana kujua kwa kuwa zimebebwa na mawimbi ya bahari hadi kuokotwa maeneo husika.

"Bahari ni pana sana na maiti hizo zinasombwa na mawimbi, hatujui zinatoka wapi, ila waulize maRPC (makanda wa polisi) wa mikoa husika."

Wavuvi waliozungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki walisema uwapo wa idadi kubwa ya miili hiyo umesababisha baadhi yao kunyamaza wanapoona miili zaidi ikielea baharini.

“Polisi tunawajulisha, wanakuja, wanabeba maiti lakini hakuna siku wametueleza ni za kina nani," alisema mvuvi mmoja wa Kunduchi aliyezungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina gazetini akihofia usalama wake.

"Wavuvi tunafahamiana na ikitokea mwenzetu amekufa au chombo kimezama majini tunafahamu.

"Lakini tangu Agosti mwanzoni tunaokota miili ikiwa imeandaliwa (imefungwa) kabisa na siyo ya wenzetu.”

Wavuvi hao walisema wamepokea taarifa kutoka kwa wenzao wa eneo la Kizimkazi, Zanzibar, kwamba huko nako pia zimeokotwa maiti tano.

Mvuvi mmoja wa Kunduchi alisema siku mbili zilizopita ziliokotwa maiti tano katika eneo la Bongoyo na nne nyuma ya kisiwa cha Mbudya, jijini Dar es Salaam.

Alisema kati ya maiti tisa hizo, moja ilikuwa ya mwanamke na kwamba zilikuwa zimefungwa kamba miguuni, kichwani na tumboni.

"Zote zilikuwa zimeharibika na sura hazitambuliki," alisema na kueleza kuwa zilichukuliwa na polisi baada ya kutaarifiwa.

Alisema polisi waliochukua miili hiyo ni wa mkoa wa Kinondoni kutoka vituo vya Kawe ambayo ni wilaya ya kipolisi na Wazo Hill.

"Hawajawahi kusema mtu huyo alifia wapi na chanzo cha kifo, (hivyo) wengi tuna wasiwasi tu," alisema mvuvi mwingine ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe.

“Ukiangalia umri ni miaka 25 hadi 50.

"Jamaa zetu wa Feli waliokota maiti sita wiki mbili zilizopita (na) kati yake mbili zimefungwa pamoja na katika hizo moja ni mwanamke.

"Tulichozoea wavuvi ni kuokota maiti za wavuvi wenzetu ambaye alizama au kupotea, na zinakuwa na nguo zake za kawaida lakini hizi ni za kuandaliwa.”



Nipashe pia iliwatafuta viongozi wa serikali ya mitaa kwenye maeneo husika, ambao walisema wamelisikia suala hilo kutoka kwa wavuvi lakini waulizwe polisi.


Chanzo nipashe
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive