MSHAMBULIAJI mpya wa Simba Mganda, Emmanuel Okwi
ametoa kauli ya kishujaa baada ya kutamka kuwa atapambana kufa au kupona
kuhakikisha timu yake inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mapema tu.
Okwi raia wa Uaganda, ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Simba
kuifunga Rayon Sports ya Rwanda kwa bao 1-0 lililofungwa na Mohammed
Ibrahim ‘Mo’ mapema wiki hii katika mchezo wa kirafiki.
Mshambuliaji huyo ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Simba, ambapo
amesajiliwa kwa dau la dola 50,000 (Sh milioni 112) kutoka SC Vila ya
Uganda.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Okwi alisema
kutokana na jinsi alivyokiona kikosi chao hadi sasa, ahadi anayoitoa kwa
mashabiki wa timu hiyo ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa.
Okwi alisema, anafurahia uwepo wa baadhi ya wachezaji wenye uwezo na
uzoefu mkubwa wa kucheza michuano ya ligi kuu na michuano ya kimataifa.
Simba itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Alisema kwa kushirikiana na wenzake, anaahidi kuipambania Simba ili
itwae ubingwa wa ligi kuu ambao mashabiki wana kiu nao baada ya kuukosa
kwa miaka mitano ukienda kwa Yanga mara tatu na Azam FC mara moja.
“Nawashukuru Wanasimba kwa mapokezi waliyonipa tangu nimetua kujiunga
na timu yangu hii niliyoichezea kwa vipindi viwili huko nyuma.
“Nimepanga kulipa fadhila kwa kuipambania timu kwa moyo mmoja kufa au kupona kuhakikisha inatwaa ubingwa wa ligi kuu mapema tu.
“Na hilo linawezekana kabisa kutokana na ubora wa kikosi chetu
tulichokuwa nacho hivi sasa, ninafurahia kuona wachezaji wenye uzoefu na
uwezo wa kupambana katika michuano ya kitaifa na kimataifa,” alisema
Okwi.
Okwi anatarajiwa kuichezea Simba dhidi ya Yanga Agosti 23, mwaka huu
katika mechi ya Ngao ya Jamii kabla ya kuanza kwa ligi kuu Agosti 26,
mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment