Monday 28 August 2017

NGOMA AREJEA KIVINGINE


Image result for ngoma yanga

DONALD Ngoma ambaye nusu ya msimu uliopita hakucheza kutokana na kuwa majeruhi, amerejea kwa kasi katika Ligi Kuu Bara baada ya jana Jumapili kutupia bao tamu la kichwa wakati Yanga ikitoka sare ya 1-1 na Lipuli.
Achana na sare hiyo, iliyopatikana Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam habari kubwa inaendelea kuwa kiungo Mkongomani Kabamba Tshishimbi ambaye pamoja na kupangiwa watu watatu, bado alifanya kazi ya maana uwanjani.
Yanga ililazimishwa sare hiyo katika mechi yao ya kwanza ya msimu, baada ya wageni wao kutangulia kufunga kupitia Seif Abdallah dakika ya 45 lakini Donald Ngoma akasawazisha sekunde chache kabla ya mapumziko.
Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Ngoma tangu alipoifungia Yanga bao la mwisho katika Ligi Kuu Februari 3 wakati walipoifunga Stand United mabao 4-0 ikiwa ni siku 205 (karibu miezi saba kamili).
Ngoma alishindwa kuichezea Yanga katika mechi za duru la pili baada ya hapo kwa kile kilichoelezwa mgomo baridi, japo mwenyewe alikuwa akidai anaumwa, lakini jana Jumapili alionekana kuhaha uwanjani kuisaidia timu isiaibike kwa Lipuli.
Hata hivyo matokeo hayo hayakuwa ishu kubwa kwa wana Yanga japo walishindwa kutoka uwanjani mapema baada ya dakika 90 wakitafakari kilichoikuta timu yao, lakini gumzo lilikuwa soka tamu la Tshishimbi aliyepangiwa viungo watatu wa kumkaba.
Katika mchezo wa jana Tshishimbi alianza kwa kasi akitibua mipango ya Lipuli ila alikumbana na changamoto ya viungo watatu wa Lipuli waliokuwa wakimtaza.
Kocha wa Lipuli, Selemani Matola aliwapanga Omega Seme, Mussa Nampaka na Shaaban Ada ambao walimbana Tshishimbi hatembei. Hata hivyo Tshishimbi aliyejiunga Yanga akitokea Mbabane Swallows ya Swaziland, alipambana kuonyesha makali yake akizima mipango ya Lipuli.
Kiungo wa Lipuli, Ada aliyeenda na Serengeti Boys Gabon mapema mwaka huu, alifanya kazi kubwa ya kumdhibiti Tshishimbi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive