Achana na habari za kuondolewa katika bodi ya wadhamini wa Simba na
kusimamishwa uanachama wa klabu hiyo huku akipewa sharti la kufuta kesi
aliyofungua mahakamani, Mzee Hamis Kilomoni hana habari na masharti hayo
na ameendelea kukomaa akisisitiza hafuti kesi.
Mkutano
mkuu wa Simba uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam iliamua
kumuondoa Hamisi Kilomoni katika bodi ya wadhamini na nafasi yake
kuchukuliwa na Adam Mgoyi huku kaimu rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah
akieleza Kilomoni kusimamishwa uanachama hadi atakapofuta kesi
mahakamani na la asipofanya hivyo watamchukulia hatua zaidi.
Kilomoni
alisema hajafuta kesi kama ambavyo imekuwa ikivumishwa na hataifuta
kesi hiyo hadi pale uongozi wa Simba utakapompelekea barua ya
kusimamishwa uanachama na kuondolewa kwenye bodi ya wadhamini.
"Nangoje
barua ya uamuzi huo, ninachojua mimi bado niko Simba kwa kuwa sijapewa
barua rasmi hadi sasa (juzi jioni)," alisema Kilomoni bila kutaka
kuzungumzia zaidi suala hilo.
"Siwezi
kulizungumzia kwa kina sababu sina barua, nitakapoletewa barua rasmi
ndipo nitakuwa katika nafasi ya kulizungumzia," alifafanua Kilomoni.
Kuhusu
taarifa za yeye kufuta kesi mahakamani, Kilomoni alisema hajafuta na
hawezi kufanya hivyo hivi sasa ingawa hakutaka kuzungumzia kama atakuwa
tayari kufuta kesi endapo ataletewa barua hiyo.
"Narudia
tena nikishapewa barua rasmi nitakuwa kwenye nafasi ya kuzungumza kila
kitu, najua klabu yetu ina matatizo mengi, lakini yote tuyaache kwanza
nisubiri barua yangu ya kusimamishwa kwanza," alisema Kilomoni.
Hata
hivyo, Simba ambayo kesho Jumapili itakuwa na mkutano wa mabadiliko ya
uendeshaji wa klabu yao mkutano utakaofanyika jijini Dar es Salaam,
uenda ikalijadili kwa mara nyingine sakata la Kilomoni.
Kaimu
rais wa Simba, Salim Abdallah alisema wanachama wa klabu hiyo wataamua
suala la Kilomoni endapo hataridhia kufuta kesi aliyofungua mahakamani.
0 comments:
Post a Comment