Monday 21 August 2017

KWELI YANGA WAMENASA KWENYE TUNDU LA SINDANO





MTEGO waliouweka Simba katika kambi yao ya wiki moja kisiwani Unguja, unaonekana kuzaa matunda kiasi ambacho hata kama Yanga ilituma mashushushu wa kuipeleleza kimya kimya wataondoka wakiwa na taarifa chache mkononi tofauti na walivyotarajia.
Simba inayorejea jijini Dar es Salaam leo Jumatatu kwa boti, benchi lake la ufundi limefanya mambo mawili ambayo yanaiumiza kichwa Yanga kutafuta namna ya kupambana nayo kabla ya timu hizo kukutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii  keshokutwa Jumatano.
Kwanza imeipa Yanga kazi ya kufahamu majina ya wachezaji watatu kati ya 11 ambao watakuwamo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba watakachokutana nacho kwenye mechi hiyo.
Hadi sasa  wachezaji wanane ambao bila shaka watakuwemo kwenye kikosi cha kwanza ambacho kitacheza na Yanga, kutokana na mechi za kirafiki na mazoezi ambayo Simba imekuwa ikiyafanya kisiwani hapa kujiandaa na mchezo huo, lakini majina matatu yamebakia kuwa siri nzito ya benchi la ufundi la Simba chini ya Mkameruni, Joseph Omog.
Wachezaji ambao wataipa ugumu Yanga kufahamu watacheza kwenye nafasi zipi keshokutwa ni Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni na Shiza Kichuya ambao wamekuwa wakichezeshwa katika nafasi tofauti tofauti mazoezini na kwenye mechi za kirafiki.
HAWA PIGA UA WAMO
Wachezaji ambao ni uhakika watacheza Jumatano labda mambo yabadilike ndani ya leo Jumatatu na kesho Jumanneni Aishi Manula, Method Mwanjali, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya, Muzamiru Yassin, Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi.
Nyota hao ndio ambao wameonekana kupewa muda mwingi wa kucheza katika mechi za kirafiki ambazo Simba ilicheza dhidi ya Mlandege na Gulioni FC lakini pia hata kwenye mazoezi ya timu hiyo, wachezaji hao wanane ndio wamekuwa wakifuatiliwa kwa umakini wa hali ya juu na benchi la ufundi.
Nafasi moja ya beki wa pembeni, moja ya ushambuliaji na ya kiungo mkabaji ndizo ambazo hadi sasa haijajulikana ni nani hasa watakaopewa nafasi ya kuzicheza katika mchezo huo.
Iwapo Simba wataamua kuanza na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ upande wa beki wa kushoto, ni wazi kuwa Erasto Nyoni atacheza beki wa kulia, lakini kama beki huyo Tshabalala hatacheza, Nyoni atacheza kushoto huku nafasi ya beki wa kulia ikichezwa na Ally Shomary.
Kwa kiungo mkabaji, Simba wanaweza kuanza na James Kotei au Jonas Mkude kulingana na mipango ya benchi la ufundi lakini pia hata Erasto Nyoni naye anaweza kucheza nafasi hiyo.
Kwenye ushambuliaji, Simba wana uhakika wa kumtumia Emmanuel Okwi kwa namba yoyote kati ya 9, 10 au 11 na hivyo kuliachia jukumu benchi la ufundi kuchagua nani aanzishwe kati ya Juma Luizio au Laudit Mavugo kulingana na mfumo.
Kingine ambacho Simba wamekifanya ni kuwachezesha baadhi ya wachezaji katika nafasi tofauti, jambo linalowapa ugumu Yanga kufahamu hasa halisi ambazo baadhi ya wachezaji watacheza siku hiyo.
Hata hivyo, kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema: “Timu ina kikosi kipana ambacho kitakuwa na faida kwetu kwenye ligi na mashindano ya kimataifa ambayo tutashiriki mwakani. Tumekuwa tukibadilisha na kuwapanga wachezaji kwenye nafasi tofauti ili kuona nani anafiti wapi na akicheza na nani.
“Mechi ya Yanga, tunaweza kumpanga mchezaji yeyote yule na tukaweza kupata matokeo kwa sababu tuna kundi kubwa la wachezaji wenye uwezo mkubwa,” alisema Mayanja.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive