Thursday 24 August 2017

KIMEWAKA JPM AAGIZA TAKUKURU KUWAKAMATA WOTE WANAOJIHUSISHA NA VITENDO VYA RUSHWA


NI rungu lingine! Licha ya mamlaka iliyo nayo kisheria, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jana ilipewa rungu lingine na Rais John Magufuli kwa kusisitizwa kuwa wamkamate yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo pasi na woga.


Aidha, Rais Magufuli ambaye tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015 amekuwa akisisitiza serikali yake kukomesha rushwa na ufisadi, aliitaka Takukuru kuhakikisha inawakamata, kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria na mwishowe kuwafunga wala rushwa wengi zaidi ili mwishowe taifa liondokane na tatizo hilo.

Katika kuondokana na rushwa ambayo baadhi ya watafiti huifananisha na kansa mbaya kwa maendeleo ya taifa, Rais Magufuli aliipa kibarua kingine Takukuru kwa kuitaka kuongeza nguvu katika kila eneo, yakiwamo yale yaliyosababisha matatizo sita aliyoyataja kama mfano kuwa vyanzo vyake ni rushwa.

Matatizo hayo ni kuwapo kwa watumishi hewa, biashara dawa za kulevya, matumizi ya vyeti feki, mikataba mibovu, ruzuku hewa ya pembejeo za kilimo na changamoto za utoaji haki mahakamani.

Rais Magufuli alisisitiza agizo lake kwa kuitaka Takukuru kuongeza makali na kuhakikisha kuwa inawakamata wanaojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa ili washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kumwapisha Brigedia Jenerali John Julius Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo.

Aidha, aliipongeza Takukuru kwa kazi iliyoanza kuifanya na kuitaka iongeze kasi yake katika uchunguzi na uendeshaji wa mashitaka ya rushwa ili vita dhidi ya rushwa ionekane ikizaa matunda haraka.

“Tukifanikiwa kupunguza rushwa kwa angalau asilimia 80, nchi yetu itafanikiwa kutatua matatizo mengi, na ni vema mtambue kuwa hatua hizi tunazochukua zimeanza kuwavutia wafadhili wengi na wawekezaji,” alisema na kuongeza:

“Na mimi nikiwa kiongozi wenu nimeamua kupambana na rushwa kikwelikweli. Na ninawaomba nyote mshirikiane kuondoa rushwa katika maeneo yenu ya kazi,” alisema.

Rais Magufuli amewataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

“Ukiangalia mambo makubwa tunayopambana nayo yanasababishwa na rushwa iliyosambaa kila mahali, watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za kulevya ndani yake kuna rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa, pembejeo za ruzuku ndani kuna rushwa na huko mahakamani nako ni rushwa tu,” alisisitiza Rais Magufuli.

AHADI YA BRIGEDIA MBUNGO

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Mbungo, aliishukuru kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine wa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.

Naye Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Harold Nsekela, aliwataka viongozi wote wa umma kuhakikisha wanajaza fomu za tamko la mali kwa wakati na pia watoe ushirikiano kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pale inapochukua hatua ya kufanya uhakiki wa taarifa zilizojazwa katika fomu hizo.

Pamoja na kula kiapo cha kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Mbungo alikula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Harold Nsekela.

Kwa upande wake, Waziri Anjellah Kairuki na Mkurugenzi wa Utawala wa Takukuru, Alex Mfungo, walimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru na kumhakikishia kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii.

Hafla ya kuapishwa kwa Brigedia Jenerali Mbungo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Mcheche Masaju.

Wengione waliohudhuria ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Anjellah Kairuki, Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba Kabudi na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive