Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Khairat Omary,
ameishtaki Hospitali ya Kairuki na kudai fidia ya Sh milioni 155 kwa
kumsababishia matatizo katika mfuko wa uzazi yaliyofanya aondolewe
kizazi.
Khairat kupitia Kampuni ya Uwakili ya
Jonas amefungua kesi ya madai namba 184 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas
Simba.
Katika madai hayo, mdai anadai
alikuwa akihudhuria kliniki wakati wa ujauzito katika hospitali hiyo na
Desemba 15 mwaka jana alijifungua kwa upasuaji, akaruhusiwa Desemba 17
mwaka huo na kutakiwa kurudi tena Desemba 21.
Mdai akiwa nyumbani alianza kusikia
maumivu ikiwamo kutapika, ilipofika Desemba 21 alirudi hospitali
akaeleza maumivu anayopata kwa daktari ambaye alielekeza afanyiwe kipimo
cha Ultra Sound.
Majibu yalipotoka daktari akampatia dawa za kutuliza maumivu na kumtaka apumzike hali itaendelea kuimarika.
“Akiwa nyumbani hali iliendelea kuwa
mbaya, alisikia maumivu makali ya kichwa na alianza kubadilika rangi
ambapo alikimbizwa hospitali ya jirani, walipompima wakaelekeza apelekwe
Regency Hospital kwa matibabu zaidi.
“Regency walimfanyia vipimo na
kubaini kuna tatizo katika mfuko wa uzazi na kumuhamishia Hospitali ya
Taifa Muhimbili ambako pia walimfanyia vipimo na kubaini wakati
alipofanyiwa upasuaji kuna vitu vilibakia kama pamba ambavyo
vimesababisha mfuko wa uzazi kuharibika,” ilisema sehemu ya hati hiyo ya madai.
Anadai ili kuokoa maisha yake
alishauriwa kuondolewa kizazi, hata hivyo licha ya kuondolewa alibakia
na tatizo la fístula lililosababishwa na pamba zilizoachwa wakati
anajifungua.
Mdai anadai kutokana na uzembe huo wa
kutokuwa makini wakati wa kumzalisha anaomba mahakama iamuru alipwe Sh
milioni 20 gharama za matibabu, Sh milioni 25 fidia kwa kukosa kipato
wakati anaumwa, Sh milioni 80 gharama za adhabu na Sh milioni 30 fidia.
Wadaiwa wanatakiwa kupeleka utete wao mahakamani na kesi hiyo itatajwa Agost 31, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment