Sunday 30 July 2017

USHINDI WA BULAYA MAHAKAMANI WATULIZA WASIRA


HATIMAYE ‘mhenga’ mmojawapo wa siasa nchini, Stephen Wasira, ameamua kutulia na kuachana jumla na kesi ya wafuasi wake kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita na kumpa ushindi aliyekuwa mpinzani wake katika jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya.


Akizungumza na gazeti la Nipashe jana, Wasira ambaye historia yake inaonyesha kuwa alianza harakati za siasa na uongozi tangu miaka ya 1970, alisema baada ya kufikia mwisho wa jitihada zake za kumpinga Bulaya mahakamani, sasa ameamua kuachana kabisa na jambo hilo na badala yake kuelekeza nguvu zake katika shughuli nyingine.

Wasira aliyasema hayo alipoulizwa kuhusiana na uamuzi uliotolewa jana na Mahakama ya Rufani wa kumpa ushindi Bulaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kesi iliyohusiana na matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015; hivyo kuwa pigo kwa kambi ya Wasira aliyeshiriki uchaguzi huo kutetea ubunge wake kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kuanzia sasa sitaendelea tena na kesi maana hapa nilipofika ndiyo mwisho… nimeona bora niangalie shughuli zangu na mambo mengine, maana hakuna namna tena kwa hapa nilipofika,” alisema Wasira, mkongwe aliyewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

Alipoulizwa kuhusu ushindi wake mwingine kortini dhidi ya mkongwe Wasira, Bulaya alisema alishamshinda Wasira kihalali jimboni na alishamtahadharisha kuwa asihangaike kwenda mahakamani maana huko nako angemshinda pia kama ilivyotokea mahakamani jana.

“Nilishamtahadharisha tangu nilipomwangusha kwamba asihangaike na kesi maana nitamwangusha tena. Lakini hakutaka kunisikia. Ona sasa… yale yale niliyomwambia ndiyo yametokea, “ alisema Bulaya na kuongeza:

“Namwomba mzee wangu Wasira asahau yaliyopita, tushirikiane kuijenga Bunda… aachane na asahau masuala haya ya kesi. Ingawa amenipotezea muda bure, namkaribisha aje tuijenge Bunda yetu.”
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive