Friday 21 July 2017

MICHAEL CARRICK ABEBESHWA ZIGO LA ROONY


Kiungo mkongwe mwenye umri wa miaka 35, Michael Carrick.
KIUNGO mkongwe mwenye umri wa miaka 35, Michael Carrick ndiye nahodha mpya wa Manchester United, amekabidhiwa majukumu hayo baada ya kuondoka kwa Wayne Rooney aliyetua Everton.
Mara baada ya kukabidhiwa majukumu hayo juzi, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Carrick aliandika: “Ninafuraha kubwa kuwa nahodha wa klabu hii, napenda kuwa hapa na nitafanya kila linalowezekana kuwa na mafanikio.”
Carrick anakuwa nahodha wa nane ndani ya United tangu kuanza kwa mfumo mpya wa Ligi Kuu England ‘Premier League’. Inawezekana akawa hana muda mrefu kuishika nafasi hiyo kutokana na umri alionao sasa, lakini tujikumbushe manahodha waliopita na mafanikio waliyopata.
Bryan Robson
Unahodha 1982-1994
Huyu ndiye nahodha aliyeshikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko wote, aliteuliwa katika nafasi hiyo na Ron Atkinson lakini aliendeleza jahazi hilo hata Sir Alex Ferguson alipoingia aliendelea kuwa naye kwenye nafasi hiyo.
Chini yake, United haikuwa na nguvu kubwa kwa kuwa ilifunikwa na Liverpool ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa na Everton miaka ya 1980, lakini alifanikiwa kutwaa taji la FA Cup mwaka 1983 na 1985.
Akielekea kuondoka, akaiwezesha United kutwaa Premier League mara mbili mfululizo mwaka 1993 na 1994 kisha akakabidhi mikoba kwa Steve Bruce ambaye alianza kushea naye unahodha mwaka 1992.
Akiongea jambo na wachezaji wa Man Utd (hawapo pichani).
Steve Bruce
Unahodha 1992-1996
Alianza kuwa nahodha baada ya Robson kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara. Alikuwa na msaada mkubwa katika ubingwa wa Premier mwaka 1996.
Bruce alibeba pia FA Cup mwaka 1994 na 1996, anasifika kwa kuwa beki mwenye kariba ya kuwa kiongozi.
Eric Cantona
Unahodha 1996-1997
Kuondoka kwa Bruce aliyetua Birmingham City mwaka 1996 kukampa nafasi Cantona kuwa nahodha kutokana na ustaa wake katika timu, ukiachana na masuala ya ukorofi pia alikuwa kiongozi mzuri.
Kilichomkwamisha kutokuwa nahodha wa muda mrefu ni kuwa aliamua kustaafu mapema akiwa na miaka 30, hiyo ilikuwa mwaka 1997, japokuwa alikuwa na mafanikio kwa kuiwezesha kutwaa Premier League katika msimu wake huo wa mwisho akifunga mabao 15.

Roy Keane
Unahodha 1997-2005
Kiungo matata ambaye alikabidhiwa kitambaa baada ya kustaafu kwa ghafla kwa mtangulizi wake, alisifika kwa kucheza soka la kupambana mwanzo mwisho.

Alikuwa nahodha wakati United inaweka rekodi ya kutwaa mataji matatu makubwa Ulaya, Premier, FA Cup na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya hapo alishinda mataji matatu ya Premier akiwa nahodha kabla ya kuondoka mwaka 2005 kutokana na kukorofishana na kocha Sir Alex Ferguson.
Nahodha mpya wa Manchester United, Michael Carrick  amekabidhiwa majukumu hayo 
baada ya kuondoka kwa Wayne Rooney aliyetua Everton.
Gary Neville
Unahodha 2005-2011
Mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea katika akademi ya United, akiwa hapo alifanikiwa kutwaa mataji 20.
Alipoteuliwa wengi waliona kama bado hajaiva lakini alikimudu vizuri kitambaa na kuwaongoza nyota wengi wakubwa wakiwemo Rooney na Cristiano Ronaldo.
Akiwa nahodha, United ilishinda Premier mwaka 2007 na 2009 na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008. Alikuwa ni mchezaji na shabiki halisi wa United. Alikuwa nahodha hadi alipostaafu mwaka 2011.
Nemanja Vidic
Unahodha 2011-2014
Alianza kupewa kitambaa kuanzia mwaka 2010 baada ya Neville kuwa majeruhi mara kadhaa, kitambaa kilimfiti kwa kuwa alikuwa na sifa kama za Neville kutokana na kujituma uwanjani na kutokata tamaa.

United ilishinda mataji mawili ya Premier chini ya utawala wake japokuwa baadaye aliandamwa na majeraha ya goti na mgongo.
Kutona na kuuguua mara kadhaa mwili wake ukapunguza nguvu ya upambanaji, mwisho akaondoka kwenda Inter Milan mwaka 2014 huku mashabiki wengi wakiendelea kumlilia.
Wayne Rooney Unahodha 2014-2017
Kuondoka kwa Vidic kukamfanya aliyekuwa kocha wa wakati huo, Louis van Gaal kumkabidhi cheo Rooney ambaye alikuwa ameshapata uzoefu wa kutosha.

Mara baada ya kukabidhiwa kitambaa, Rooney alibadilika kitabia, akaacha ukorofi na muda mwingi akawa kiongozi japokuwa alikuwa na wakati mgumu kwa kuwa timu iliyumba kutokana na kuwa katika kipindi cha mpito.
Chini yake mataji yalikuwa haba lakini ukame huo uliisha mwaka 2016 kwa kutwaa taji la FA Cup, licha ya kufunga mabao mengi kuliko wenzake kikosini bado ilikuwa ngumu kutwaa ubingwa wa Premier.
Akiwa nahodha pia aliweka rekodi ya kufunga mabao mengi na kuwa mfungaji bora wa klabu hiyo akimzidi Bobby Charlton aliyekuwa akishikilia rekodi kwa miaka mingi.
Baada ya kuingia kwa Kocha Jose Mourinho, nafasi yake ikawa finyu na mwisho ameamua kuondoka kwenda Everton akiwa na mafanikio ya kutwaa Kombe la Ligi (EFL Cup) na Kombe la Europa pamoja na Ngao ya Jamii ambavyo vyote walivichukua msimu uliopita.
Michael Carrick
Unahodha 2017- Tangu atue United mwaka 2006 akitokea Tottenham Hotspur, hakuwa maarufu wala mtu wa kutajwa na mashabiki wengi lakini kazi yake huwa ni kubwa, umuhimu wake ulionekana miaka ya hivi karibuni pindi alipoanza kupigwa benchi na makocha kadhaa wa kikosini hapo ambao walihisi uwezo wake ni wa kawaida.
Lakini licha ya umri kuwa mkubwa bado amekuwa na umuhimu kikosini na inawezeka amepewa unahodha ili awe kama kocha mchezaji japokuwa anaweza hasicheze michezo mingi.
Carrick
Urefu: Futi 6 inchi 2
Namba ya jezi: 16

Timu
1999-2004: West Ham
1999: → Swindon (mkopo)
2000: → Birmingham (mkopo)
2004-2006 Tottenham
2006-sasa Man United

Timu ya taifa England
2001–, mechi 34, mabao 0
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive