Marekani imesema kuwa itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini ''iwapo ni lazima'' kufuatia jaribio la kombora la masafa marefu lilotekelezwa na taifa hilo.
Balozi wa Marekani Nikki Haley alisema kuwa maamuzi mapya pia yatawasilishwa dhidi ya Pyongyang katika Umoja wa Mataifa.
Alielezea jaribio hilo kama tishio la kijeshi mbali na kutishia kutumia vikwazo vya kibiashara.
Jaribio hilo la kombora , ambalo ni la hivi karibuni miongoni mwa majaribio mengine linakiuka marufuku ya baraza la Umoja wa Mataifa.
Wakati huohuo waziri wa ulinzi nchini humo James Mattis na mwenzake wa Japan Tomomi Inada walisema kuwa jaribio hilo ni uchokozi ambao hautakubalika.
Taarifa iliotolewa na wizara ya ulinzi imesema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu ambapo Jenerali Mattis alisema Marekani itaendelea kuilinda Japan.
Bi Haley alisema siku ya Jumatano kwamba jaribio la kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini ICBM linaangamiza suluhu ya uwezekano wa mazungumzo ya kidiplomasia
''Marekani imejiandaa kutumia uwezo wake wote kujilinda na washirika wetu'', aliambia baraza la usalama katika Umoja wa Mataifa, ambalo lilikutana kwa kikao cha dharura kuzungumzia hatua hiyo ya Korea Kaskazini.
''Moja ya uwezo wetu upo katika jeshi. Tutautumia iwapo ''tutalazimika'' kufanya hivyo ,lakini tungependelea kutoelekea upande huo'',alisema.
Bi Haley ambaye alisema alijadili swala hilo na rais, alisema kuwa Marekani pia inaweza kukata biashara na mataifa ambayo yanaendelea kufanya biashara na Korea Kaskazini kwa kukiuka maamuzi ya Umoja wa Mataifa.
''Tutayaangazia mataifa ambayo yanaendelea kufanya bishara na utawala huu usiofuata'' sheria ,alisema.
0 comments:
Post a Comment