Amri Athman ‘Mzee Majuto’ akiugulia.
MWEZI Mei, mwaka huu, gazeti ndugu la hili, Ijumaa Wikienda liliripoti habari mbaya juu ya lejendari wa vichekesho Bongo, Amri Athumani 'Mzee Majuto' kuwa katika hali mbaya kiafya, lakini kwa hali yake ilivyo kwa sasa anahitaji dua za Watanzania.
AFANYIWA UPASUAJI
Habari mbaya zilizolifikia Amani, mapema
wiki hii zilieleza kuwa, Mzee Majuto yu kitandani kwa mara nyingine
kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa uliosababisha afanyiwe upasuaji.
Chanzo makini kililieleza Amani kuwa,
Mzee Majuto ambaye amezaliwa mwaka 1948, alilazwa kwa siku tano
hospitalini huko mkoani Tanga akisumbuliwa na ugonjwa wa hernia (ngiri)
ambapo ililazimu afanyiwe upasuaji ili kumsaidia kwenye tatizo lake hilo
la muda mrefu.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, kufuatia
tatizo hilo, Mzee Majuto amekuwa akitumia dawa za hospitalini na zile za
kienyeji, lakini hakuna unafuu wowote anaoupata.
“Kuna kipindi alilazwa hapo katikati,
alipopata nafuu aliruhusiwa lakini wiki iliyopita alibanwa sana na
unajua yule mzee alikuwa anaogopa kufanyiwa operesheni ila kutokana na
afya yake imebidi akubali tu,” kilisema chanzo chetu hicho na kuongeza:
“Kimsingi Mzee Majuto anahitaji dua za mashabiki wake na Watanzania kwa jumla.”
Mzee Majuto.
MKE WA MZEE MAJUTO AFUNGUKA
Baada ya kupata habari hizo, Amani lilimtafuta
msanii huyo kwa njia ya simu yake ya kiganjani ambapo ilipokelewa na
mkewe, Aisha Yusuf ambaye alithibitisha mumewe kuumwa.
Mama Majuto alisema kuwa, hadi wakati
anazungumza na gazeti hili alikuwa yupo na mumewe katika Hospitali ya
Tanga Central Health Centre (TCHC) ambako alilazwa kwa siku tano na
kufanyiwa upasuaji.
“Ni kweli Mzee Majuto anaumwa ndiyo
maana nimepokea simu yake, nipo naye hapa hospitalini, anasumbuliwa na
ugonjwa wa hernia ambao umeibuka na kumuanza tena.
“Tunamshukuru Mungu kwa sasa anaendelea
vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji hivyo Watanzania na mashabiki wake
waendelee kumuombea na Mungu akipenda hivi karibuni tu atarudi mzigoni,
watarajie mambo mazuri kutoka kwake,” alisema mama Majuto.
Amani lilipoomba kuzungumza na Mzee Majuto mwenyewe, mkewe alisema alikuwa usingizini kwani alitakiwa apumzike baada ya upasuaji.
“Nitamfikishia pole lakini haruhusiwi kuzungumza, anatakiwa kupumzika,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Hata hivyo, tumeambiwa tutaruhusiwa kutoka hapa hospitalini muda wowote.”
MASHABIKI WAMMISS
Wakiongea na gazeti hili, baadhi ya
mashabiki wa staa huyo walisema kuwa, wamemmiss sana kwenye fani yake ya
uigizaji na kumuomba Mungu afanye miujiza na amrejeshee afya yake.
“Kwa kweli tumemmiss sana, tunaamini
atapona na kurejea kwenye hali yake ya kawaida,” alisema mmoja wa
mashabiki aliyejitambulisha kwa jina la Said Juma.
UGONJWA WA HERNIA
Hernia au ngiri ni aina ya ugonjwa
ambao humpata mtu baada ya misuli au kuta za tishu mwilini
zinazoshikilia au kubeba viungo (organs) fulani kupoteza uimara au kuwa
na uwazi (opening) hivyo kusababisha viungo hivyo kutoshikiliwa
ipasavyo.
Miongoni mwa vitu vinavyoweza
kumsababisha mtu kupata hernia ni pamoja na kuwa na uzito mkubwa au
kuongezeka uzito kwa ghafla, kazi ya kubeba au kunyanyua vitu vizito,
tatizo la kukohoa au kupiga chafya kwa muda mrefu, ujauzito au matatizo
yanayojitokeza kwa mwanamke wakati wa kujifungua.
Pia kuharisha au kuvimbiwa
(constipation). Vitu hivyo humfanya mtu apate hernia ambayo husababisha
afanyiwe upasuaji ili kumaliza tatizo hilo.
CHANZO: AMANI
0 comments:
Post a Comment