Tuesday, 25 July 2017

JAJI WAREMA AFAFANUA KAULI YAKE JUUN YA KAFULILA


 Mjadala mkali wa sakata la uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ulisababisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema kutumia msemo unaomtaja tumbili wakati akimjibu mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila.


Werema alijitokeza jana kufafanua kuhusu kauli yake, lakini mjadala huo wakati huo ulikuwa na matamko tofauti wakati joto bungeni lilipozidi, likigawa wabunge na hata viongozi wa Serikali.

Katika hotuba yake akiwa jimbo la Kigoma Kusini juzi, Rais John Magufuli alifufua tena mjadala huo wakati alipompongeza “kwa dhati” Kafulila kwa uzalendo wake wa kuibua kashfa hiyo iliyohusu Sh306 bilioni na kusimamia kutetea hoja yake hadi mwisho.

Rais alisema Kafulila alipata shida hadi baadhi walimuita tumbili, neno lililotamkwa na Werema wakati akijibu mwongozo wa mbunge huyo wa Kigoma Kusini, na kwamba waliomuita hivyo sasa wamegeuka tumbili.

“Lazima niwe mkweli na nisiposema hapa nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu, siku zote ukweli utabaki kuwa ukweli tu na ndiyo maana nampongeza Kafulila kwa sababu alisimama imara kupigania maslahi ya umma. Alionyesha uzalendo wa hali ya juu unaopaswa kuigwa na kila mmoja wetu,” alisema Rais.

Jana, Werema alimwambia mwandishi wetu kuwa alisema neno hilo kama msemo wa Kiswahili. Mwandishi wetu alipomuuliza kuhusu kauli ya Rais juzi, Jaji Werema alijibu:

Jaji Werema: Sasa unataka nifanyeje?

Mwandishi: Tunahitaji maoni yako kuhusu kauli hii.

Jaji Werema: Hilo jambo si liko mahakamani? Tunaweza kushtakiwa, wako mahakamani?

Mwandishi: Sawa. Lakini kwa kipindi kile kati ya watu ambao walimuita Kafulila tumbili, wewe ni mmoja wao.

Jaji Werema: Unajua wengi walishindwa kuelewa nilisema nini, mimi nilichokizungumza ni kwamba tumbili haamui mambo ya msituni, na huo ni msemo wa kawaida tu.

Kafulila, ambaye alikuwa mbunge wa Kigoma Kusini kuanzia 2010 hadi 2015 kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, aliibua kashfa hiyo bungeni baada ya kuisoma katika gazeti la The Citizen mwaka 2014.

Kwenye sakata hilo jumla ya Sh306 bilioni zilichotwa kutoka akaunti hiyo iliyofunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL baada ya kutokukubaliana katika tozo ya uwekezaji.

Baada ya Kafulila kuanzisha mjadala huo, Bunge liliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi na taarifa yake ilitumiwa na chombo hicho cha kuisimamia Serikali kujadili kwa kina uchotwaji wa fedha hizo.

Licha ya kwamba wabunge wa CCM waliungana na upinzani katika sakata hilo, mjadala ulitawaliwa na mihemko na ushabiki na haikuwa ajabu kwa Werema kujikuta akitoa kauli hiyo.

Kila mbunge aliyesimama kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika, ukumbi ulikaa kimya kusikiliza lakini aliposimama mbunge aliyetetea kuwa fedha za escrow hazikuwa za umma kulikuwa na kelele za kumpinga na za kumshangilia, kiasi cha kulazimisha kiti cha spika kutuliza hali kila wakati.

Wakati Bunge lilipofikia kuweka maazimio, kikao kilifanyika hadi saa 5:00 usiku bila ya kufikia muafaka na kulazimika kuahirisha hadi siku iliyofuata kutoa nafasi kwa wabunge kujadiliana maazimio.

Miongoni mwa hoja zilizotolewa kukuza tatizo hilo ni zile zilizotolewa na mbunge wa zamani wa Nkenge (CCM), Assumpter Mshama, ambaye alidai kuna watu wengine waliopewa fedha wakiwa Mombasa nchini Kenya, na kumtaja mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa mmojawao.

“Hata mheshimiwa Mbowe amediriki kutajwa kwamba alipokea pesa kule Mombasa, lakini humu hakuna taarifa zake. Taarifa za benki ya Stanbic hatujasikia taarifa zake, lakini wanaojulikana wamepata pesa ni wa CCM. Ndio maana tunasema hata kama hiyo kamati ya PAC,” alisema huku sauti ikitaka kutoa taarifa.

Mshama alitakiwa atoe ushahidi kuwa Mbowe alitoa fedha lakini alishindwa na baadaye kufuta kauli yake.

Mwingine aliyetetea kuwa fedha hizo hazikuwa za Serikali ni mbunge wa Magomeni (CCM), Mohamed Chombo aliyewatuhumu walioshupalia suala hilo kuwa walikuwa na uchu wa madaraka.

“Sasa hivi, VIP imenunuliwa na PAP. Inabidi yeye-- kwa maana ya PAP-- alipe fedha zake za hisa parcent (asilimia) 30. Fedha hizi baada ya kutoka, PAP inabidi amlipe VIP. Sasa ndugu yangu nataka niwaambie--sasa nataka kuja kwenye ile ashki majinuni ni nani,” alisema.

“Kuna watu ambao maisha yao yote, wao ni watu wenye ashki. Ashki ni hamu ya kutaka na wao wapate kila wanachokipata wengine. Kuna watu wana ashki ya kupata madaraka haya.”

Credit - Mwananchi
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive