Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amesema muda si mrefu atatoa majibu ya suala la mauaji yanayotokea mkoani Pwani.
IGP Sirro amesema hayo
leo (Julai 5) wakati wa makabidhiano ya magari manne ya polisi
yaliyotolewa msaada na Kampuni ya Great Wall Motors and Haval.
“Si kawaida yangu kusemasema ila muda
si mrefu nitatoa majibu ya mauaji ya Pwani. Sisi Watanzania hatujazoea
mambo ya fujo fujo, wale waliotumwa kwa ubaya ubaya sisi tunawajibu
vibaya vibaya,” amesema IGP Sirro.
Tangu Mei mwaka jana yalipoibuka mauaji
ya kutumia risasi katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani
Pwani, takriban watu 37 wameuawa wakiwamo askari polisi na viongozi wa
Serikali za Mitaa.
Kamishina wa Polisi Kitengo cha Fedha
na Usafirishaji, Albert Nyamuhanga amesema magari hayo yenye thamani ya
Sh120 milioni kila moja, yatasaidia kupambana na uhalifu nchini.
“Kupatikana kwa magari haya kumeokoa
fedha nyingi katika bajeti ya Serikali, hivyo wadau hawa wameunga mkono
juhudi za polisi kukabiliana na uhalifu,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Great Wall Motors
and Haval, Jianguo Liu amesema magari hayo ni pongezi kwa kazi
inayofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi.
“Tunaunga mkono juhudi za polisi za kutunza amani na usalama wa raia,” amesema Liu.
0 comments:
Post a Comment