Dar es Salaam. Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali maombi ya marejeo ya
aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Mbagala kwenye Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015, kupitia CUF, Kondo Bungo.
Kondo alifungua maombi ya marejeo mahakamani hapo akipinga uamuzi wa
Mahakama Kuu kuwaondoa mashahidi wake watatu katika orodha kwenye kesi
yake ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo, kutokana na viapo vyao
kuwa na kasoro za kisheria.
Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake imetupilia mbali maombi hayo, baada
ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na wajibu maombi, kuwa
hayana mashiko kwani yanakiuka sheria kwa kuwa wametumia kifungu ambacho
kinazuia kukata rufaa na kuomba marejeo kwa mambo ambayo ni ya uamuzi
usiomaliza shauri mahakamani.
Kwa uamuzi huo, sasa kesi hiyo inasubiri kupangiwa tarehe ya kuendelea
kusikilizwa mashahidi wengine wa mdai katika Mahakama Kuu.
0 comments:
Post a Comment