Sunday, 1 January 2017

BURIANI OFISA MTENDAJI MKUU WA WAKALA WA NDEGE ZA SERIKALI



OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan Mhaiki, amefariki dunia jana saa 5:25 asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es Salaam.

Alilazwa katika hospitali hiyo Alhamisi iliyopita, kabla ya sikukuu ya Krismasi, kwa ugonjwa wa saratani ya ini.

Kaka mkubwa wa marehemu, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Sheria, Oliver Mhaiki alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na HabariLeo.

Mhaiki alisema Kapteni Keenan ambaye ameendesha marais wa awamu zote tano, alianza kuumwa Julai mwaka huu kwa kusumbuliwa na pingili ya ‘lumber’, hali iliyoelezwa na madaktari ni kwa sababu ya kukaa muda mrefu.

Alisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na maumivu na Oktoba mwaka jana alipokwenda India kwa ajili ya uchunguzi zaidi, ndipo baadaye alirudi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

“Kilichomuua sio hicho, inaonekana alikuwa na saratani ya ini muda mrefu, hakuigundua, hivyo wiki mbili zilizopita alibadilika rangi kuwa njano, alipoenda hospitali wakagundua ni saratani,” alisema kaka huyo wa marehemu.

Alisema marehemu ameacha mke na watoto wawili na kwamba anatarajiwa kuzikwa Songea. Alisema hivi sasa wanasubiri wadogo wa marehemu waliopo nje ya nchi.

Alisema katika familia yao, wamezaliwa watoto nane.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive