Beki wa kati wa Simba, Mganda, Juuko Murshid.
MPANGO wa Yanga kukamilisha usajili wa beki wa kati wa Simba, Mganda, Juuko Murshid, hatimaye umeyeyuka baada ya mabosi wa Msimbazi kumuwekea ngumu.
Hiyo ni siku chache tangu ziwepo tetesi za Yanga kumfuata beki huyo
nchini Uganda kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ili wamsajili msimu
ujao wa Ligi Kuu Bara.
Yanga hivi sasa ipo katika mipango ya kuiimarisha safu yake ya ulinzi
baada ya beki Mtogo, Vincent Bossou kuondoka kutokana na kushindwana
maslahi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano kutoka ndani ya uongozi wa Simba, beki huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja kwa ajili ya kuichezea Msimbazi.
Mtoa taarifa huyo alisema, Simba haina mpango na beki huyo kutokana
na yeye mwenyewe kugoma kurejea kujiunga na timu hiyo huku ukipanga
kumuuza sehemu yoyote lakini siyo Yanga.
Aliongeza kuwa, Simba na Yanga hazina ujamaa wa kuachiana wachezaji
kutokana na utani wa jadi uliopo kwenye klabu hizo kongwe na pinzani.
“Juuko bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba, licha ya kutokuwa na
mpango naye, lakini hatutakubali kumuachia aende kuichezea Yanga msimu
ujao.
“Na ikumbukwe kuwa Simba na Yanga hazina ujamaa wa kupeana wachezaji
kirahisi, tena akiwa bado ana mkataba, niseme tumeweka makubaliano kuwa
kama mchezaji anataka kuondoka Simba, basi aende kwingine lakini siyo
Yanga, labda mkataba wake uwe umemalizika.
“Hivyo, kama Yanga wanamtaka Juuko wasubirie hadi msimu ujao akiwa
mchezaji huru lakini msimu huu kujiunga na timu hiyo haitawezekana,”
alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna kuzungumzia
hilo simu yake ya mkononi iliita na baadaye kukatwa, gazeti hili
halikuishia hapo liliendelea kumtafuta Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
timu hiyo, Said Tully, simu yake iliita na yeye akakata.
0 comments:
Post a Comment