MARTHA MAGAWA
Leo tutazungumzia juu ya mambo ya
kuzingatia kama unahitaji kudumu katika uhusiano ulionao. Hapa naomba
nizungumze na wanawake zaidi.
Nasema hivyo kwa sababu wao ndiyo wanaokumbana zaidi na matatizo ya kuachwa na wapenzi wao kuliko wanaume.
Ni sahihi kusema, wanawake ndiyo
huumizwa zaidi katika mapenzi kuliko wanaume. Hii ni kutokana na sababu
kubwa mbili kwa kawaida wao ndiyo hufuatwa na kutongozwa na wanaume,
lakini lingine ni kwamba, mara nyingi wanaume ndiyo hutoa uamuzi wa
kuacha au kuachana.
Kwa sababu hizo, hakuna ubishi kuwa wanawake ndiyo walengwa wakubwa wa
mada hii, Rafiki zangu, kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanaweza
kusababisha uhusiano kuwa butu na baadaye kuishia njiani.
TAMBUA THAMANI YAKO
Ili uweze kuwa bora ni lazima uanzie kwako, ujitambue kama mwanamke na
thamani yako kwa mwanaume wako. Ukiijua thamani yako, lazima utakuwa
makini na kila kitu, Uamini kwamba wewe ni mwanamke mrembo na
unayevutia. Imani hiyo ikishaingia, tayari utakuwa unajali mambo mengi
ya msingi, ikiwemo usafi wako binafsi. Waswahili wanasema, mwanamke ni
pambo la nyumba.
Kwamba nyumba bila mwanamke haiwezi
kukamilika, wewe kama mwanamke unatakiwa kufahamu wewe ni kila kitu
ndani ya nyumba. Umakini wako na kujitambua ndiyo vitu vitakavyokuweka
katika nafasi nzuri ya kudumu katika uhusiano wako na baadaye kuingia
kwenye ndoa.
TAMBUA THAMANI YAKE
Ukiijua thamani ya mwanaume kutoka ndani ya moyo wako ni wazi kwamba
hata vipengele vifuatavyo hapa chini havitakuwa vigumu kwako
kutekelezeka. Inakupasa ujue thamani ya mwanaume wako ipasavyo.
Hilo si tu kwa maneno, bali ni jambo
ambalo linatakiwa kufanyika kwa ridhaa ya moyo wako. Ni rahisi zaidi
jambo hili kufanyika ikiwa utakuwa na mapenzi ya dhati. Mpende kwa moyo
wako wote na ujue kuwa maisha yako yanakamilishwa na uwepo wake.
MHESHIMU
Mwanaume anapenda sana kuheshimiwa na mpenzi wake. Mwanaume akigundua
haheshimiwi au unafanya hivyo kwa kumridhisha tu na si kutoka moyoni, ni
rahisi kukuacha.
Kama kichwa cha familia, lazima apewe
nafasi ya kutoa uamuzi tangu mapema. Ikiwa utakuwa na majibu mabaya
kwake, humheshimu ni wazi kwamba atakuacha mapema, maana utakuwa
umepoteza sifa za kuwa mama wa familia.
SOURCE: MTEMBEZI
0 comments:
Post a Comment