BY Brown Mgeni
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitangaza mkakati wa chama
hicho kufanikisha mikutano na maandamano ya walichokiita Umoja wa
Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), huku jeshi la polisi nao wakijiandaa
kukabiliana nao.
Mbowe aliitaja mikakati hiyo ikiwamo kamati za kuhamasisha Ukuta ambapo
aliyekuwa mgombea urais kupitia Ukawa Edward Lowassa amepangiwa Mbeya,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji atakuwa Mwanza, Makamu
Mwenyekiti Profesa Abdallah Safari atakuwa Tabora huku Mwenyekiti wa
Bawacha Taifa, Halima Mdee na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere
Marando wakipangiwa Dar es Salaam.
Alisema yeye (Mbowe) ataongoza Kanda ya Kaskazini wakati Profesa Mwesiga
Baregu amepewa jukumu la kufafanua Ukuta kwa taasisi za kimataifa,
viongozi wa dini na wastaafu.
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu na mawakili 12 wao watajifungia Dar es Salaam kufungua kesi 21 kutetea mikutano.
Lakini, Jeshi la Polisi limesema litatoa taarifa rasmi baadaye huku CCM wakisisitiza msimamo wao wa kupinga maandamano hayo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema jeshi hilo
litatoa taarifa siku chache zijazo. “Tutawaita na tutazungumza, naomba
tujaribu tu kuvuta subira,”alijibu kwa ufupi msemaji huyo wa polisi.
Hata hivyo kikosi cha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika
mikoa mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam na Kilimanjaro walionekana
wakifanya mazoezi wakiwa na silaha na magari ya maji ya kuwasha kwa siku
tofauti.
CCM watoa ushauri
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema licha ya chama
kuzungumza mara kadhaa, wanatarajia kutoa tamko kwa lengo la kuwaeleza
Watanzania tahadhari juu ya mchezo unaojaribiwa na Chadema.
Sendeka alisema viongozi wa dini na makundi mbalimbali yameshauri juu ya mipango yao, lakini hawataki kusikia.
“Jambo hilo limezungumzwa mara nyingi sana, viongozi wa dini
wameshasema, watu wenye mapenzi na nchi yao wakishauri waache huo mchezo
wao ambao sidhani kama watafanikiwa, kwa hivyo tunatarajia kutoa tamko
letu siku yoyote kuanzia kesho (leo),”alisema.
Mbowe na safu yake
Akizungumza wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Chadema Kanda ya
Kaskazini jana katika Hoteli ya Coridol Springs jijini hapa, Mbowe
alisema chama hicho kimejipanga kufanya mikutano na maandamano ya amani
nchi nzima Septemba Mosi ili kutetea utawala wa sheria na Katiba.
Mbowe alisema Rais Magufuli aliapa kuilinda Katiba, Wabunge waliapa
kuilinda Katiba, madiwani waliapa kuilinda Katiba ili nchi iongozwe
katika misingi ya sheria na utawala bora.
Alisema haiwezekani nchi kuongozwa kwa matamko ambayo yanakiuka katiba
na Chadema kama chama kikuu cha upinzani kina wajibu wa kuishauri na
kuikosoa serikali na hawawezi kukaa kimya.
Alisema matamko ya Rais kuwa hakuna ruhusa ya kufanya mikutano ya
kisiasa kwa vyama vingine na kuacha chama chake kufanya mikutano na pia
kuzuia mikutano hadi mwaka 2020 haikubaliki.
“Sisi tunataka nchi iongozwe kwa kufuata sheria na siyo matakwa ya
viongozi ambayo yanakinzana na sheria na Katiba ya nchi,” alisema Mbowe.
Alisema wanafanya mikutano na maandamano kama sehemu ya kueleza
malalamiko yao, hasa kutokana na kauli za viongozi ambazo zinakiuka
sheria.
Mbowe alisema vyama vyote vikiamua kukaa kimya na kuacha mambo
yaliyotokea Zanzibar, yaliyotokea Dodoma na yanayotokea sasa kutokana na
kauli za viongozi, ni wazi nchi haitakuwa salama.
“Tukiamua sote kujifanya wanafiki kusema hewala nchi haitakuwa salama
itazaa taifa la watu wenye hofu na ndiyo sababu tumeamua kamati kuu
kuanzia sasa kufanya kazi kila siku kuisaidia sekretarieti,” alisema.
Mbowe alisema kutokana na unyeti wa Ukuta, Kamati Kuu ya Chadema imeunda
kamati ndogo tano, ambazo zitasaidia kufikiwa malengo yaliyokusudiwa
kwa kuhusisha taasisi na vyombo vingine.
Alisema pia kuna kamati ya maandalizi ya Ukuta ambayo tayari imeanza
kazi ya kufafanua maamuzi ya kamati kuu, ambayo sasa imesambaa katika
kanda zote kutoa elimu kwa viongozi wa Chadema.
“Katika kanda zote nchi nzima viongozi watakwenda kuzungumza na
wanachama wa kada zote na kuwaelimisha kwanini Kamati Kuu imefikia
maamuzi ya kuanzisha Ukuta kabla ya kushiriki mikutano na maandamano
Septemba Mosi,” alisema
0 comments:
Post a Comment