Thursday, 14 April 2016

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yapongezwa Kwa Kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 Kwa Amani




Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala imeipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kufanikisha kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 vizuri na kuiacha nchi ikiwa na Amani, utulivu na Usalama.

Hayo yalisemwa jijini Dar ess Salaam jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh Najma Murtaza Giga walipokutana na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere convention Center katika kikao mahsusi cha Kupitia Bajeti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Aidha, pongezi hizo kwa NEC zilitolewa na wajumbe wa pande zote mbili yaani wa Chama tawala na wale wa upinzani wa kamati hiyo kwa nyakati tofauti.

Baadhi ya wabunge hao ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa Najma Murtaza Giga(CCM), Twahir Awesu Mohammed (CUF) na Nassor Suleiman Omar (CUF).

Alisema ni jambo la heri sana pale ambapo taasisi ama mtu anafanya kazi ya kutukuka kupewa sifa yake na kupewa moyo ili aendelee  na moyo wa kufanya kazi kwa bidii na hatimaye kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi  si tu kwa manufaa ya taasisi yake bali hata kwa Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhan aliiambia kamati hiyo kwamba haikuwa  kazi rahisi kuendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Nchi ikaendelea kuwa na amani na utulivu kwani ushindani wa kisiasa ulikuwa mkubwa kiasi cha kutishia maisha ya watanzania.

“Tulijitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kufuata Sheria Kanuni na taratibu za kusimamia Uchaguzi pamoja na kwamba Bajeti ilikua haitoshi hasa wakati tunaanza zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura kwa kutumia Teknolojia ya BVR ambapo tulilazimika kuandikisha wapiga Kura kwa kuhamahama” Alisema Kailima.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge Jenista Mhagama aliwashukuru wabunge kwa niaba ya Serikali kwa jinsi walivyothamini na kutambua Kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuahidi kufikisha Serikalini mawazo ya kuitafutia Tume fedha kwaajili ya Tume kuzipatia Asasi za Kiraia zinazotoa Elimu ya Mpiga Kura kwani lilijitokeza suala la Ukosefu wa Fedha za Kuendeshea Elimu hiyo.

Bajeti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 ni jumla ya Tsh 4,830,537.167/= ikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida OC Miradi ya Maendeleo pamoja na Mishahara ya watumishi.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulifanyika tarehe 25 Oktoba ambapo aliyekua Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Mh.Dkt John Pombe Magufuli aliibuka Mshindi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Ads

Blog Archive